|
Tunahitaji biblia ili kupata Kweli ya Rohoni,
lakini ili kuielewa,
Mungu yule aliyewaongoza waandishi,
lazima awaongoze na wasomaji pia.
Ukurasa huu unatafiti
mistari
ili kujifunza jinsi ya
kuondoa
ukungu unaopelekea kuzuia mafunuo ya kiroho,
ili tusiingie katika upotofu.
Kwa nini Wakristo wazuri wanapojifunza mistari ile ile ya biblia, na kuwa na uhakika kuwa wamepata Kweli ya Mungu, huishia kuwa na tafsiri [yaani Mungu anamaanisha nini] zinazopingana?
Ni ukweli unaotisha na kushangaza pale kutokukubaliana katika kutoa maana ya mistari ya biblia kunatokea hata kwa wale Wakristo waliobobea, waliojazwa na Roho Mtakatifu au hata wataalamu wa thiolojia.
Sote tunaamini tunatafsiri kwa usahihi neno la Mungu lakini tafsiri zetu zinazokinzana zinaonesha kuwa pengine sisi sote tumetafsiri kimakosa kwa kiasi fulani sio kama upotofu, lakini Mungu wetu tunayemtumikia siye Mungu wa iliyo Kweli? Tafsiri yoyote isiyo sahihi inaweza pelekea matokeo yasiyofurahisha.
Ombi langu ni kuwa ukurasa huu uwe ni rahisi kueleweka. Kwa sababu topiki hii ni muhimu sana kwa Wakristo wote. Ninakiri lengo kuu ni kuweka tofauti moja. Nitalileta neno moja hermeneutics ambalo ni geni kwa wasomaji wengi japo linajulikana sana na wachungaji, wanathiolojia au hata wanafunzi wa shule za Biblia. Katika kutafiti ukurasa kama huu, watu hao watatafiti maana ya neno hermeneutics katika mitandao. Kwa hiyo kwa kulihodhoresha hapa kwa mara kadhaa, itasaidia kuelewana. Wengi wetu ambao tunatumia lugha ya kawaida ni muhimu sana kwangu na kwa Mungu pia. Hermeneutics inazingatia msaada wa kielimu katika kutafsiri Biblia kwa usahihi kwa kuzingatia mazingira, kuelewa kipindi wakati mistari hiyo inaandikwa, na kadhalika.
Mimi ninaamini katika hermeneutics nzuri. Nimeandika kitabu kidogo kuhusiana na hiyo. Kwa kuendelea kusoma ukurasa huu, utazidi kuwa na uhakika kwamba, japo hermeneutics ni muhimu, Biblia inatufundisha kwamba mambo muhimu katika kutafsiri biblia kwa usahihi ni ya kiroho, sio kielimu.
Mmoja anaweza toa hoja kwamba hermeneutics inayofundishwa katika vyuo vya thiolojia ni hermeneutics ya kielimu Kanuni za kutafsiri Biblia ambazo Wakristo na wasio Wakristo wanaweza kuzitumia vizuri. Huu sio ukosoaji: Mungu ni wa busara. Ametuumba tukiwa na uelewa, na cha muhimu zaidi ni kwamba sheria zake zinatutaka tumpende yeye kwa kutumia kila kitu ndani yetu, ikiwemo akili zetu. Kutafsiri Biblia kwa kutumia elimu pekee haitoshi kwa sababu Yesu mwenyewe alisema:
Yohana 4:24 Mungu ni roho, na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho . . .
Mathayo 13:11 . . . Ninyi mmejaliwa kuzifahamu siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.
Mathayo 16:23 . . . Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya Mungu bali ya binadamu.
Yohana 8:43-44 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu mnakataa kusikiliza ujumbe wangu. Ninyi ni wa baba yenu shetani . . .
Na katika maneno ya Paulo:
Warumi 8:7 . . . wenye mawazo yaliyotawaliwa na mambo ya mwili ni adui wa Mungu. Watu kama hao hawakubali kutii sheria ya Mungu, na kwa kweli hawawezi.
1 Wakorintho 2:12-14 Sisi hatukupokea roho ya dunia hii bali Roho aliyetoka kwa Mungu ili tuweze kuelewa kuelewa yale ambayo Mungu ametupatia bure. Haya ndio tunayozungumzia, lakini si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, nasi tunafafanua mambo ya kiroho kwa watu wa kiroho. Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yanayotokana na Roho wa Mungu . . . na hawezi kuyaelewa kwa kuwa hayo yanaeleweka tu kwa msaada wa Roho.
Kama hermeneutics ya kielemu ilivyo ya umuhimu, ukurasa huu utazingatia ambayo nitaiita hermeneutics ya kiroho kuelewa ukweli wa mambo kiroho katika biblia kwa njia ambayo Wakristo tu wanaweza kuipata na/au kuielewa. Kama sentensi hiyo inakushtua, sitashangazwa.
Inaonekana kama haijakamilika lakini tutagundua kuwa hii ndio njia ambayo imesisitizwa mara kwa mara katika Maandiko kitabu ambacho chanzo chake ni rohoni. Tutagundua pia hii sio dalili ya maazimio yasiyokamili au matamko yasiyo na ushahidi.
Badala yake, ni wito wenye akili kwa ajili ya wacha-Mungu, wenye furaha, wanaomtegemea Muumbaji na Hakimu kwa ajili ya ufunuo na uelewa.
Tunajua ya kwamba mungu wa dunia hii ametia giza akili za wasioamini (2 Wakorintho 4:4). Sio kwamba wana upungufu wa akili, au hata ufahamu. Wasioamini wako chini ya uzuizi wa rohoni ulio endelevu ambao unawafanya wasiielewe kweli ambayo ingewaweka huru. Lakini kuwa mwamini inamaanisha mwisho wa mashambulizi hayo?
Je tuna maono ya 20/20 ya papo kwa hapo kuhusu kila kweli ya rohoni chini ya anga? Ni Zaidi ya hatua za mwanzo humfanya mpanda mlima kufika kilele cha Mlima wa Everest. Ilikuwa ni kwa waamini waliojazwa na Roho Mtakatifu ambao Paulo aliwaandikia:
Waefeso 1:17-18 kwamba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni roho ya hekima na ya mafunuo mpate kumfahamu zaidi. Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yaangaziwe ili mpate kujua tumaini mliloitiwa na mtambue utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watu wa Mungu . . .
Hawa ni watu wale wale ambao Paulo alisema tayari wako ndani ya Kristo (Waefeso 2:6) na waliokuwa wamebarikiwa . . . na kila baraka ya rohoni zitokanazo mbinguni ndani ya Kristo (Waefeso 1:3). Pamoja na hadhi yao ya kiroho na ufahamu wa kiungu, Paulo alijua kwamba kama Wakristo walihitaji mafunuo zaidi. Zaidi sana na hii itatushangaza baadhi yetu alijua ya kwamba hata barua zake na hata kusoma sana visingetosha kutoa mafunuo ambayo wangehitaji. Alijua jambo la muhimu la kufanya ili wapokee uelewa wa rohoni ni maombi endelevu kwa ajili ya mafunuo hayo.
Wakati wanathiolojia wote hawakujua kuhusu kuzaliwa kwa Masia wao, wachunga kondoo walipokea mwaliko wa kiungu kwenda kumwabudu mtoto Yesu. Kumbukumbu za Mbinguni zimejaa na Habari za aina hiyo.
Yesu alimfurahia Mwenyezi alipoficha siri zake kwa wale wenye hekima [machoni pao wenyewe na/au machoni wa ulimwengu]. Badala ya kuwafunulia kweli za rohoni kwa wenye ujuzi wa thiolojia, Bwana wa mabwana alichagua kuwaumbua wale waliojisifia akili zao kwa kuwafunulia kwa maksudi siri za rohoni kwa wale ambao hawakwenda shule.
Upende usipende, Mungu ni Mungu. Anaamua nini afunue na kwa nani.
Mathayo 11:25 Wakati huo Yesu alisema, Ninakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, na ukawafunulia Watoto wachanga . . .
Wenye hekima na wenye elimu Yesu aliowaongelea hawakuwa watu wasiomjali Mungu bali ni watu ambao maisha yao yote yalihusika katika kumtumikia Mungu na kujifunza kwa undani kabisa Neno lake. Walikuwa ni wahitimu wa shule ya biblia, wanathiolojia na wahubiri walioheshimika kipindi hicho ambao walikuwa wametiwa sumu na akili zao wenyewe na kujitoa kwao ambao Mungu aliwaacha waendelee kuwa vipofu, na kwa maksudi kuwafunulia siri zake za rohoni kwa watu wa kawaida.
Hili ni Andiko kuu:
Yohana 9:39-41 Yesu akasema, Nimekuja ulimwenguni kutoka hukumu; ili wale walio vipofu wapate kuona; na wale wanaodhani wanaona, waonekane kuwa vipofu. Baadhi ya Mafarisayo waliomsikia akisema hiviwakauliza, Je, unataka kusema kuwa sisi pia ni vipofu? Yesu akawajibu, Kama mngekuwa vipofu kweli, hamngekuwa na hatia,. Lakini kwa kuwa mnasema Tunaona, basi bado mna hatia. . . .
Elimu kubwa ya Biblia na ujuzi wa kithiolojia waliokuwa nayo Mafarisayo, ambayo ilitakiwa kuwa msaada mkubwa, ilipelekea kuwa kikwazo. Inasemekana elimu ndogo ni hatari, lakini uhalisia wa kutisha ni kuwa, elimu zaidi ni hatari zaidi kwa sababu inaongeza uwezekano wa kupofushwa na majivuno na kupelekea kutofundishika.
Yakobo anagusia katika hili:
Yakobo 1:22 Basi muwe watendaji wa neno na wala msiwe wasikilizaji tu, ambao wanajidanganya wenyewe.
(Msisitizo ni wangu)
Ni kweli kwamba, kujifunza Biblia ni muhimu sana, lakini pale ambapo msisitizo zaidi unapowekwa kwenye kujifunza Maandiko kuliko kuyaishi, udanganyifu ni rahisi kutokea.
Kuna wale ambao Biblia kwao ni muongozo wa Maisha na wale ambao Biblia kwao ni fasihi ya kusisimua. Biblia ni barua ya upendo ambayo huwafanya baadhi kupekelea kumpenda zaidi Mwandishi. Kwa wengine, ni barua tu ya upendo.
Wale wanaoweza hufanya; wasioweza, hufundisha, ni jambo baya ambalo huweza kutokea. Si ajabu Yakobo aliandika:
Yakobo 3:1 Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.
Biblia ni ramani itumikayo kwa msaada mkubwa na wasafiri wa rohoni na sio wale wasiosafiri japo wanajisikia fahari kuweza kuisoma hiyo ramani.
Kila mchezo una mabingwa wake na una mashabiki wake ambao hujiskia fahari kuwa na ujuzi sana kuhusu mchezo husika. Je unataka kuwa nani katika mchezo wa maisha?
Tafakari mtu ambae elimu na ujuzi wake kuhusu Biblia ni mdogo mno na bado kwa kidogo anachojua amepiga hatua kubwa kiroho kuliko profesa wa seminari. Ni nani kati ya hao ambae Mungu anamuona ni mjinga?
Jibu ni kwamba, sio kujifunza kidogo Biblia, bali ni kuiishi zaidi.
Kwa nini? Kupata ufahamu zaidi? Hapana. Mzaburi anaendelea:
Lengo lake lilikuwa si kushinda mchezo wa kujua habari nyingi za Biblia. Lengo lake la Biblia lilikuwa ni kujifunza kutomkosea Mungu. . . . Usiniache nipotee mbali na maagizo yako aliomba (Zaburi 119:10)
Tena tunasoma:
Yoshua 1:8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku.
Kwa nini?
. . . upate kuangalia kutenda kulingana na maneno yote yalioandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapostawi sana. (Msisitizo ni wangu)
Yoshua aliamriwa kiungu kusoma sana Maandiko sio kwamba awe na elimu zaidi bali ili aweze kuyaishi.
Na tena tunasoma:
Kumbukumbu la Torati 29:29 Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na Watoto wetu milele . . .
Kwa nini?
Katika mfano wa Yesu wa mtu aliyejenga Maisha yake juu ya mchanga na yule aliyejenga juu ya mwamba, wote walijua mafundisho ya Yesu (Mathayo 7:24-27). Walitofautiana sio katika elimu ya mambo ya rohoni. Ilikuwa ni nini walifanya na elimu hiyo kilichotofautisha hatima zao.
Ni kanuni ya kiroho kwamba yule aliye mwaminifu na kidogo, atapewa zaidi (linganisha Mathayo 24:46-47; 25:21). Wale ambao hawachukui hatua ya kufanyia kazi kweli za kibiblia wanazofahamu tayari, si rahisi kumfanya Mungu awafunulie kweli zaidi. Mafunuo zaidi yatawafanya wawajibike zaidi, hivyo kupelekea kupata hukumu zaidi.
Tulimsoma Yesu akiwaambia Mafarisayo, Kama mngekuwa vipofu, mngekuwa hamna dhambi, lakini sasa mwasema, Twaona. Basi dhambi yenu yakaa . . . Kungekuwa na tumaini kubwa kwao kama wangekuwa na unyenyekevu wa kugundua ni jinsi gani uelewa wao ulivyo mdogo.
Kila mkristo anajua kwamba japokuwa Mungu anatamani kusamehe dhambi zote, kwa Mwokozi wetu kufanya hivyo, tunatakiwa kutambua kwanza tu watenda dhambi. Vivyohivyo, Mungu anatamani kufunua macho yetu ili kuona kweli za rohoni lakini tunatakiwa kwanza kutambua upofu wetu. Daktari wa macho anaweza akawa tayari kurekebisha tatizo letu la macho bure, lakini mikono yake imefungwa kama tukikataa kutambua kuwa tunahitaji msaada wake au tunaona tutajishusha hadhi kwa kuvaa miwani.
Kukubali kuwa na upofu wa kiroho ni adimu na ni vigumu kwa mtu ambae ana elimu na ujuzi mkubwa wa Biblia. Biblia si tatizo. Ni mtazamo wa mtu. Ni ngumu sana kwa mtu ambae ana elimu ya mambo ya rohoni kubwa sana kupiga hatua katika ufalme wa Mungu kwa sababu ni ngumu kwa mtu huyo kugundua ni kwa kiasi kidogo tu ndicho anachofahamu na ni jinsi gani anahitaji msaada wa kiungu katika kuielewa Biblia.
1 Wakorintho 8:2 Mtu akidhani anajua neno, hajui lolote bado, kama impasavyo kujua.
Ni sawa na kuwa na maadili mazuri mno na kujitoa kwingi. Ilikuwa ni kwa watu wenye maadili mazuri ambao Yesu alisema, watoza ushuru na makahaba wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu (Mathayo 21:31).
Tunatakiwa tusilegeze kujitoa kwetu kwa Mungu na kujifunza Neno lake. Kama tukianza kufikiri kwamba ufunguo wa kuwa na uelewa wa kiroho ni juhudi zetu kuliko neema ya Mungu, tupo kwenye hatari kubwa na kuwa na upofu wa kiroho. Inakuwa ni sawa na sungura na kobe, wale wenye elimu ndogo ya Biblia kuwapita wanathiolojia.
Lazima tujifunze kwa mwandishi wa Zaburi 119. Elimu na ujuzi wake wa Neno la Mungu ulikuwa ni mkubwa na bado alikuwa ni mnyenyekevu wa kuomba kuwa na uelewa zaidi na kumsihi Mungu asimfiche maana halisi ya Maandiko ambayo kila mtu alijua mwandishi huyo anayafahamu zaidi kwa undani. Huyu ni mtu ambae aliutafuta moyo wa Mungu; mtu ambae hakuruhusu elimu yake kubwa kukwamisha ukuaji wake kiroho.
Alikuwa yuko katika mstari sahihi na Mungu kiasi kwamba alitumika kuandika Andiko, mzaburi aliomba, Usinifiche maagizo yako (Zaburi 119:19).
Kama Mwenyezi akiamua kuficha kweli, hata wenye akili nyingi au wana hermeneutics bora waliopo duniani hataweza kufichua. Na yeyote anayefikiri hawezi kuanguka katika upotofu huu tayari ameshadanganywa.
Kwa jinsi ambavyo mbinu za kielimu zilivyo muhimu, zinafifia kwa umuhimu ukilinganisha na wingi wa mbinu za kiroho katika kuielewa na kutafrisi Biblia.
Kwa kujumuisha ukweli huu kwa maneno machache:
Tunapotafuta ukweli wa mambo ya rohoni ,
Biblia ni lensi ya Mungu.
Hatuwezi kuona sawasawa bila hiyo.
Lakini Mungu ni mwanga.
Bila yeye hatuoni kitu.
Bado sijadangwa (ila nina uhakika shetani analifanyia kazi) kiasi cha kufikiria mimi si rahisi kuanguka nikilinganisha na Wakristo wengine. Ombi langu ni kwamba, kwa pamoja tugundue sababu zote za kwa nini Wakristo wanakuwa na mahitimisho yanayokinzana (na hivyo kuonesha kuwa baadhi yetu hutuko sahihi) tukitafiti kwa kudhamiria kweli kutoka katika Biblia ileile. Ni wazi kuwa, lengo la ukurasa huu ni kujifunza kupunguza uwezekano kwa makosa haya ya kiroho. Hamna jambo la umuhimu zaidi ya hili, na bado ni topiki ambayo inaonekana kusahaulika.

Mipaka ya Ufahamu
Sifikiri kwamba vyuo vyote vya Kikristo vimeingia katika mtego huo, ila wanavutiwa zaidi kuweka msisitizo katika kutoa mafunzo ya ufahamu/akili kuliko ukweli kwamba tafsiri sahihi ya Biblia ni jambo la kiroho kama ilivyo maombi au kupokea mafunuo na maelekezo ya kiungu. Jaribio lolote la kufanya njia ya elimu ya darasani pekee kuwa chanzo cha kutafsiri Biblia litaishia kufeli.
hermeneutics inachukuliwa kama sayansi ya kutafsiri Biblia. Moja ya mambo muhimu ya sayansi ni kuwa, jaribio au uchunguzi ukifanywa kwa kurudiwa na watu tofauti, matokeo yaleyale yanapatikana. Hii haitokei katika biblia kwa sababu, tafsiri sahihi ya Biblia sio sayansi tu bali inategemea na uhusiano kati ya viumbe viwili sisi na Mungu.
Nilifunza sayansi ya kitabia (utafiti wa saikolojia) kipindi cha ujana wangu, na sayansi kwa ujumla imeendelea kunifurahisha. Katika suala la kutafsiri Biblia, neno sayansi linatakiwa kuamsha umakini, likituonya kwamba hili ni jaribio la kupandikiza uelewa wa kisasa wa kimagharibi katika suala la kiroho ambalo Mungu aliwapa wanadamu hata kabla ya sayansi ya kimagharibi kuwepo. Japokuwa nyakati zinabadilika, bado tunaishi katika kipindi ambacho wanadamu wanatekwa na nguvu ya ufahamu wa kibinadamu kuliko mambo ya rohoni. Na Wakristo hawana kinga na kuenea kwa mtazamo huu ambao hupelekea uharibifu wa kifikira.
1 Wakorintho 3:18-19 Mtu asijidangaje mwenyewe, kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao.
Tafsiri ya Biblia iliyo sahihi, haipatikani kama ua lililokufa lililobanwa katikati ya kurasa za Biblia. Tafsiri sahihi ya Biblia inapatikana kupitia uhusiano ulio hai mawasiliano ya kiundani na Mwandishi Mkuu. Kweli ya kibiblia inapatikana kwa kumjua mtu, kwa sababu Kweli ni mtu Bwana Yesu Kristo. Ninapenda sana kusoma lakini ni muhimu kutoruhusu njia ya kielimu ya kujifunza Biblia kuchukua nafasi ya kujifunza kupitia ukaribu wa kiroho na Mungu. Hiyo itakuwa ni kama kufanya mahaba kuwa maswala ya kikemia. Tafsiri sahihi ya Maandiko ni kitu cha ndani kama kuhisi pumzi ya mtu umpendae kwenye shingo yako anapokushirikisha siri zake za ndani.
Japo inawachukiza wale ambao hujivunia akili na uelewa wa akili zao, Biblia ni Neno la Mungu na ni yeye ambae huamua ni nani ataelewa anachomaanisha. Kwa kuwa Mungu ni upendo, anachothamini sio uelewa wa akili za kibinadamu au hata kujifunza sana bali ni ukaribu wao kwake. Kwa hiyo anasukumwa kuwazawadia uelewa wa Neno lake sio wale wanaotafiti sana Biblia kwa kuongeza ufahamu tu, bali wale wanajiofunza kumtafuta yeye.
Waebrania 11:6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
Mathayo 6:33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
Yeremia 29:13 Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
(Msisitizo ni wangu.)
Kwa kutaka wewe umtafute kwa moyo wako wote; Mungu kidogo ni kama msichana ambaye humzungusha kijana anayempenda sana, akitumaini itakufanya uendelee kumpenda zaidi.
Kama mtu anayekupenda atafanya juhudi kubwa kukuandikia barua, haitaleta heshima kutoisoma barua hiyo kwa umakini mkubwa, lakini pia itavunja heshima kutotambua uwepo wake akikutembelea na kuendelea tu kusoma barua.
Maisha ya milele sio kujua Biblia bali ni kumjua Mungu. (Yohana 17:3). Amri kuu sio kupenda Neno la Mungu bali ni kumpenda Mungu mwenyewe. Ndio, kama ukimpenda Mungu utalipenda Neno lake, lakini unaweza kupenda kujifunza Biblia pasipo kumpenda Mungu.
Ndio, ni muhimu kusoma Biblia ukiwa na lengo la kuliishi, na sio lengo tu la kujua sheria au kutimiza jukumu linalochosha bali lengo liwe kwa ajili ya hamu ya kumjua Mungu zaidi, Mpenzi wa maisha yako na kumfurahisha. Tunatakiwa kusoma Neno la Mungu kama ambavyo mtoto mdogo anayetamani kukua na kuwa kama Baba yake; kama kijana aliyejawa na hisia za mahaba anapofungua barua yake ya kwanza kutoka kwa mpenzi wake; kama ambavyo mama anaposoma barua kutoka kwa mwanae aliye vitani, akitamani kujua kama kuna analomaanisha zaidi ya alichoandika; kama mwanafunzi ambaye haridhiki kufikiria peke yake maana ya kitabu husika, bali humuuliza maswali mara kwa mara mwalimu ampendaye.
Bwana huficha maana ya Neno lake kama siri inayolindwa vizuri kwa wasomaji wa juujuu tu, kwa sababu anatamani upendo wako.
Mwandishi wa Biblia anatamani usomaji wa Biblia uwe ni kwa wakati wa kipekee, maalumu uliotengwa, yaani mawasiliano ya pande mbili. Anataka tuje kusoma Biblia sio kwa kuuliza tu, Ni nini mwandishi anataka kuwaambia watu wake? bali Ni nini unataka kuniambia sasa Bwana? Ni rahisi kuingia katika mawasiliano ya ndani wakati wa kusoma Biblia kwa kuuliza maswali kama, Ninashangaa hiki kinamaanisha nini? Je kinamaanisha hivi? Kinyume chake, Mungu anatamani sisi kulifanya liwe maombi, tukisema maneno kama, Je hiki kina maana gani Bwana? Asante kwa kweli ya kipengele hiki. Nisaidie kufanyia kazi mstari huu. Nisamehe kwa jinsi mstari huu unavyonihukumu kuwa ni mkosaji.
Usisome tu Biblia bali omba kupitia Biblia. Uje kwa Biblia sio kwa kujifunza tu bali kuongoza maisha yako ya maombi kukupa mambo ya kuombea wakati unaongea na Mungu. Tafiti Maandiko sio kwa ajili ya ufahamu tu, bali kwa ajili ya moyo wako. Matokeo hayatakuwa tu ya kufurahisha na kutosheleza bali itamgusa Mungu kukushirikisha yaliyo moyoni mwake kwako, akikufunulia Neno lake kwako kwa njia ya kipekee na sahihi zaidi.
Kuachana na hermeneutics itakuwa ni makosa, lakini hata hermeneutics iliyo bora haitoshelezi. Ndiyo maana Maandiko hayatupi sisi masomo kupitia hermeneutics bali yanatoa msisitizo katika mambo ya rohoni na moyoni. Ni kweli kwamba, moja ya mambo yanayowachangaya wasomi wa Biblia wa sasa ni kwamba mara nyingi hata waandishi wa Maandiko hawakufuata kanuni za kutafsiri Biblia zinazopendekezwa na wanathiolojia wa sasa!

Umepofuka Kiasi Gani?
Fikiria wayahudi ambao Yesu aliwaambia:
Yohana 5:39-40 Mnayachunguza Maandiko kwa sababu mnadhani ndani yake ninyi mna uzima wa milele; na maandiko yayo hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
Baadhi ya hawa wanafunzi wa Neno walitaka Yesu afe. Hata baada ya kufufuka kwake, wengi wao waliweza soma Agano la Kale kwa umakini mkubwa lakini wasiweze kuelewa kuwa Agano hilo la kale lilikuwa linamdhihirisha Yesu kuwa ni Masiya wao. Tunapenda kujiona sisi ni wa kiroho zaidi kuliko wao kama wao walivyojiona ni wa kiroho zaidi ya wale waliowaua manabii. Kiuhalisia, pamoja na matamko yetu kuwa tumejazwa na Roho Mtakatifu, kama kumbukumbu zetu zingeondolewa hadi kubaki na taarifa ambazo hawa Wayahudi walikuwa nazo Agano la Kale na baadhi ya taarifa kuhusu Yesu, bila maelekezo yoyote wengi wetu, kama wao, tungepitwa (tusingeelewa) na jinsi Yesu alivyokuwa anatimiza Maandiko.
Ni wangapi kati yetu, kwa mfano, wangeona mauaji ya watoto yaliyofanywa na Herode Bethlehemu au mtoto Yesu alivyokimbilia Misri au alivyokulia Nazareth kuwa ni utimizwaji wa Maandiko (Mathayo 2:14-23)? Tungekuwa tumefundiswa katika hermeneutics ya kisasa, ni dhahiri kabisa tungepitwa na mambo mengi ya Agano la Kale yaliyomwelezea Yesu. Hatuna tofauti na wale Wayahudi, vipofu wa kiroho kama tunavyodhani.
Roho Mtakatifu anaweza kuwa Mwalimu wetu, lakini hii inamaanisha mwisho wa ujinga wa kiroho si zaidi kama kuingia kwenye chuo cha udaktari kunamfanya mtu awe bingwa wa upasuaji. Ni kwa kiasi gani tunamsikiliza Mwalimu wetu? Ni kwa kiasi gani tunafuata maelekezo yake? Ni kiasi gani tunafanya mambo yetu wenyewe au kujaza fikira zetu na maelekezo kutoka kwa walimu wa hadhi ya chini?
Kutafsiri Neno la Mungu kwa usahihi ni jambo la kiroho kama kumtegemea Roho Mtakatifu kama mwandishi wa mwanzo kabisa wa Biblia.
2 Petro 1:20-21 Mkijua neno hili kwanza, hakuna unabii katika Maandiko upatao kutafsiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali binadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
Biblia ni kitabu chenye asili ya uungu, kilichopangwa kueleweka na wale ambao wanaweza kupata vya rohoni.
Bila hermeneutics nzuri, tungekuwa nje ya mstari ki-hadithi lakini bila kuangaziwa binafsi rohoni tungekuwa tumepotea kabisa. Biblia ni ramani yetu; Roho Mtakatifu ni mwongozaji wetu. Upana wa ramani ni mkubwa mno tunahitaji mwongozaji. Mwongozaji anaongea taratibu kiasi kwamba tunahitaji ramani kuhakikisha kuwa tumesikia kwa usahihi. Bila umakini wa karibu kwa vyote viwili (ramani na mwongozaji), tutapotea. Hii sio kwa sababu ya upungufu wa chochote kati ya hivyo. Ilikuwa imepangwa sikuzote kuwa vyote vifanye kazi pamoja.
Mnapotea, kwa kuwa hamyajui Maandiko wala uweza wa Mungu alikemea Yesu. (Mathayo 22:29). Tunavimba kwa kiburi. Onyo la Yesu halituhusu! Aliendelea kusema kuwa Mungu kumwambia Musa, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo inaonesha kwamba wafu hufufuliwa. Ni nani ambaye angengamua hilo kutoka kwenye Andiko hilo?
Kuhusu wale wayahudi ambao kusoma kwao sana Biblia kuliwafanya wasiwe Wakristo, Paulo aliandika:
2 Wakorintho 3:14-16 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; ila hata leo, Torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. But their minds were
Wale waliokosea kabisa katika uelewa wao wa Maandiko hawakupungukiwa akili wala elimu. Ni kweli, walikuwa bora zaidi katika idara zote mbili kuliko Wakristo wengi. Kama Paulo alivyoandika:
1 Wakorintho 1:19-29 Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi mwandishi? Yuko wapi mleta hoja wa nyakati hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuuzi wa lile neno lililohubiriwa . . . si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; . . . Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima . . . ili mwenye mwili awaye tote asije akajisifu mbele za Mungu.
Haikuwa akili wala elimu, bali ukuta wa kiroho uliowafanya Wayahudi hawa wasiione Kweli.
1 Wakorintho 2:9-14 lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu . . . Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho . . . Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi ili tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu . . . Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. (Msisitizo ni wangu)
Tumeona kwamba, Roho anatolewa ili tujue (1 Wakorintho 2:12) and Matendo 5:32 inatuambia Roho anatolewa kwa wale wanaomtii Mungu. Ukweli huu unajumuisha kile ninachoona ni jambo la muhimu alilotamka Yesu:
Yohana 7:17 Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu.
Yesu anasema kwamba endapo Mungu atampa mtu uwezo wa kiungu kuelewa asili ya mafundisho ya Yesu, inategemea utayari wa mtu huyo kufanya mapenzi ya Mungu. Tunaona hili likiwa limesisitizwa tena sehemu nyingine:
Ezekieli 12:2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi.
Ona uhusiano mkubwa uliopo kati ya uasi (kukataa/kuzuia mapenzi ya Mungu) na kutoweza kuona na kusikia ukweli wa mambo ya rohoni. Hii inaelezea vizuizi vinavyozuia uelewa wa mambo ya kiroho. Je tuko tayari kulipa gharama yoyote ili tufanye mapenzi ya Mungu? Ni kwa kiasi gani tutachagua kujikana nafsi, tukitoka jasho kama vile ya matone ya damu, huku tukilia si mapenzi yangu, bali yako na kisha kubeba msalaba wetu na kumfuata Bwana hadi kwenye kifo cha mateso kwa ajili ya Mungu? Hilo kwa kiasi kikubwa litaamua ukaribu Mungu atakaotuweka na ukweli wa mambo ya rohoni.
Ni kwa sababu tafsiri ya Biblia iliyo sahihi sio zao la ujuzi wa kielimu bali ni la mafunuo ya kiroho, ndiyo maana tuna Maandiko kama:
Kumbukumbu la Torati 29:4 lakini Bwana hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi.
Isaya 29:10-11 Kwa maana Bwana amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu; yaani waonaji. Na maono yote, yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri . . .
Mathayo 13:10-16 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mfano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyanganywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia . . .
Tunaendelea kushawishiwa kutozingatia maonyo ya Maandiko kama vile yanamhusu mtu mwingine, na sio sisi, ni kama vile kuwa Wakristo inatupa kinga ya kupotoshwa au upofu wa kiroho. Katika hayo aliyosema Yesu hapa juu, tungeweza fikiri kuwa wanafunzi hawangeweza kuja kuwa na moyo mgumu. Hata hivyo, walikuwa ni wateule wa Kristo; wachache ambao walipewa kujizua siri za Ufalme wa Mbinguni Ilikuwa ni wengine ambao walikuwa na macho yasiyoweza kuona na masikio yasiyoweza kusikia ukweli wa mambo ya rohoni, si ndiyo? Soma tena:
Marko 8:17-18 . . . Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho hamwoni; mna masikio, hamsikii? . . .
Hata kama tuko karibu sana na Yesu na kubarikiwa sana mambo ya rohoni, haimaanishi kuwa hatutaweza kamwe kuanguka katika upofu wa kiroho ambao utatufanya tusione kweli za mambo ya rohoni ambayo tunatamani sana kuyajua.
Kuwa wasikiao wasioelewa ni jambo la kutisha, hasa inapokuwa inaongelea kuhusu ukweli wa mambo ya rohoni na sio jinsi ya kutumia DVD kinasa. Na lilitokea sio kwa wale ambao hawakupata elimu bali kwa wasomi wa Biblia walio wengi wa Israeli. Kupata elimu ya darasani ni jambo la muhimu, lakini kutafsiri Biblia ni suala na kiroho la ndani mno kiasi kwamba moyo na roho ya mtu ni muhimu zaidi kuliko akili zake. Fikiri, kwa mfano, maana ya Maandiko yafuatayo:
Marko 6:51-52 Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito. [Kwa maneno mengine, mioyo yao mizito ilizuia wao kuelewa ufunuo uliopita kuwa Yesu alikuwa ni nani hasa.]
Luka 24:45 Ndipo akawafunulia akili zao [ilibidi Mungu aingilie kati], wapate kuelewa na Maandiko.
Yohana 16:13-14 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote . . . Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.
Yesu alifundisha kwa mifano ambayo iliwapumbaza wasikilizaji. Ni kama hilo halikuwa halitoshi kupoteza wafuasi, alifanya pia na mambo ambayo yaliwaudhi wale waliojaribu kusimamia Maandiko. Kwa mfano, machoni pa wengi alionekana kuvunja kwa makusudi moja ya Amri Kumi kwa kuchagua mara kwa mara kuponya siku ya Sabato (ambayo ingeisha wakati wa jua kuzama) badala ya kusema, Rudi baada ya saa chache. Alisema kwa kujua mambo ya kuudhi bila ya kujisumbua kujielezea, mfano, aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele (Yohana 6:53).
Njia ya Yesu ya ufundishaji haikupingana na ya Mungu. Yesu alikuja kudhihirisha moyo wa Baba na alifanya hivyo hata katika ufundishaji wake. Kama yalivyo mafundisho ya Yesu, Mwenyezi ameifanya kwa maksudi Biblia nzima iwape shida wasomi na kuwa rahisi kukosewa katika kuitafsiri na kuielewa. Ni Dhahiri, kitovu cha Ukristo msalaba ni kama:
1 Wakorintho 1:23 bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulubiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi
Bwana wetu kwa makusudi anafanya ukweli ya mambo ya rohoni na hata wokovu kuwa ni kosa kwa wale wanaojivunia akili au kutokukosea. Anafanya hivi kwa sababu anatamani sisi tuwe halisi kama inavyodhihirishwa na ukweli na unyenyekevu wetu na anatamani ukaribu na sisi. Ni kwa imani, ukweli na unyenyekevu, na sio akili za kuzaliwa au kujitosheleza kunakoleta majivuno, ambayo anayaheshimu.
Wakati Petro anatamka kuwa Yesu ni Masiya, Mwana wa Mungu, Yesu alisema kuwa ufunuo huo uliomfikia Petro haukutoka kwa wanadamu bali ulitoka kwa Mungu mwenyewe (Mathayo 16:17). Hiyo ndiyo asili ya ufunuo. Haitokani na nyama na damu, wala akili na kusoma bali hutoka kwa Mungu. Ufunuo wa kweli wakati wote unaendana na Maandiko na mara nyingi unakuja kupitia Maandiko hasa kujifunza sana Maandiko lakini unatokana na tafsiri ya Roho ya Maandiko, sio jaribio la kibinadamu katika kutafsiri.
Kwa kuwa Biblia ni Neno la Mungu, sio letu, ni haki yake kulitumia jinsi yoyote aipendayo. Imekuwa ni tabia ya Bwana wetu unaweza sema ucheshi wake kumfunulia mtu wa kawaida ukweli wa thamani ambao mwana thiolojia ameukosa kabisa, na cha kushangaza pengine kuudhi kwa makusudi msomi kwa kumruhusu yule mtu wa kawaida agundue ukweli (tafsiri sahihi) kwa kuchukulia/kuelewa Maandiko nje ya mstari.
Tunaweza tusiabudu sanamu za mawe, lakini ni kwa wasomi wangapi na/au Wakristo waliokomaa Andiko hili linawahusu, Wakijinena kuwa wenye hekima, walipumbazika (Warumi 1:22)?
Mbele za Mungu huyo, ninaweza anguka kwa kumwabudu, nikimwambia
Warumi 11:33-34 Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake?

Kuta Zinazozuia Ukweli wa Rohoni
Moja ya vitu vinavyonishawishi kuwa Injili (vitabu) ni za kweli ni kwamba kama wanafunzi mashuhuda wa habari yenyewe wangekuwa na tabia ya kupindisha ukweli, wangejiandika kwa jinsi ambayo wangeonekana bora zaidi. Hawa wanahabari waliruhusu si tu kutoonekana wa maana bali pia kwa kuiweka katika lugha nzuri ni kama vile akili zao hazikuwa nyingi. Tunawaona wakigombana kwa mambo madogo na kuonywa mara nyingi na Yesu kwa kuwa wa imani ndogo pia tunawaona wakiwa hawakuelewa mifano mpaka Yesu alipoielezea zaidi walipokuwa pekeyao. Kinachoonekana kwao ngumu kuelewa ni kwamba Yesu alikuwa akiendelea kuwaambia kuwa atateswa na kufufuliwa kutoka kwa wafu, jambo ambalo hawakulielewa. Hii haizungumzwi tu katika kila Injili, bali pia imesisitizwa sio mara moja ila zaidi ya mara mbili katika Injili moja:
Luka 9:22 akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka
Wiki moja hivi baadae, Yesu alisema:
Luka 9:44-45 Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katka mikono ya watu. Lakini hawakufahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.
Sura tisa baadae, Yesu alikuwa bado akiwafundisha kuhusu kuteswa kwake na uelewa wao ulikuwa bado mbovu.;
Luka 18:31-34 Akawachukua wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. Walakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa. They understood (Msisitizo ni wangu)
Ni katika Luka pekee, hii ni mara ya saba Yesu alikuwa ameongea kuhusu kuteswa kwake mbeleni (Mistari). Bila shaka ugumu wao ulikuwa ni kuelewa kwamba Yesu wakati huu alikuwa anaongea kwa lugha ya wazi (bila kificho). Japo kutokuelewa kwao ni muhimu sana kwetu kwa sababu kama hawa wateule wa Mungu waliweza kukosa kweli ya mambo ya rohoni, na kwetu pia hii hali inaweza kututokea. Katika ukurasa unaofuata tutaendelea kujifunza suala hili muhimu.
I M E E N D E L E Z WA Ukurasa Unaofuata (English only)
Afrikaans Webpages
 Not to be sold. © Copyright, Grantley Morris, 2005, 2017. For much more by the same author, see www.net-burst.com These writings may be freely copied provided they are not placed in a webpage, nor in anything that is sold and provided this entire paragraph is included. For use outside these limits, written permission is required. Freely you have received, freely give.
[Other Topics] [E-Mail Me!]
[Bless & Be Blessed by Facebook] [Daily Quotes] [My Shame]
|
|